WAKATI SAHIHI NI SASA
by Humphrey W. Mrema
Katika vitu ambavyo huwa napenda kuvifanya na vinanijenga kimaarifa ni kusoma vitabu na magazeti. Nakumbuka ilikuwa tarehe 17 mwezi wa Sita, mwaka 2021. Siku hii huwa ni maadhimisho ya kimataifa ya kupambana na ukame duniani. Nilikuwa nasoma gazeti mojawapo ambalo katika moja ya habari iilikuwa na kichwa kinachosema “Ukame wasababisha kupungua kwa nyumbu Hifadhi ya Taifa Serengeti.” Mimi kama mdau wa masuala ya mazingira na mabadiliko ya tabia nchi nilivutiwa na nikawa na shauku ya kusoma habari hii. Sehemu mojawapo ya habari hii ilinukuu maneno haya “Ilipofika mwaka 1977 kulikuwa na nyumbu takribani milioni moja na laki nne (1,400,000). Aidha, ukame mkubwa uliotokea mwaka 1993 ulisababisha vifo vya wanyama wengi na kupunguza idadi ya nyumbu hadi kufikia laki tisa na kumi na saba elfu (917,000).” Habari hii ilinishtua na kunijengea hamu ya kutamani kujua jinsi gani ukame uliosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi ulivozorotesha idadi ya wanyama na viumbe hai duniani kiujumla.
Nilijifunza mengi sana kupitia vitabu na kwa njia ya mtandao ni kwa jinsi gani mabadiliko ya tabia nchi yameharibu shughuli nyingi za kibinadamu na hata kuhatarisha uwepo wa viumbe wengi katika sayari yetu. Rafiki yangu mmoja aliwahi kuniambia kuwa “suala la mabadiliko ya tabia nchi halijaacha mtu, kila mmoja, kila jamii, kila nchi, kila bara, dunia yote kwa namna moja au nyingine inaathirika na mabadiliko haya.” Kauli yake hii ilifungua akili yangu na nikaelewa kuwa, kila mmoja anapaswa kuwa balozi wa kulinda mazingira maana madhara yanayokuja katika karne hii huenda yakawa ni ya kwanza na ya hatari zaidi kuwahi kutokea katika sayari yetu na historia ya Ulimwengu mzima.
Katika kuendelea kujifunza, siku moja kwenye taarifa ya habari, kwenye habari za kimataifa nikasikia wananchi wa kule Ufilipino wanafanya ibada ya kuombea ndugu zao waliopotea na wale waliofariki kutokana na kimbunga cha Yolanda kilichoipiga nchi yao pamoja na maeneo mengine ya jirani mwezi Novemba, mwaka 2013. Inasemekana zaidi ya watu millioni 11 waliathirika na kimbunga hichi, maelfu walifariki, makumi elfu walipoteza makazi na wengi wao hadi leo wamepotea na hawajulikani walipo. Inaumiza, tena inaumiza sana! Lakini je! Kiini cha tatizo hiki ni kipi? Ni wazi kuwa mabadiliko ya tabia nchi ni kichocheo kikubwa cha madhara haya yaliyoandikwa kwenye historia ya dunia.
Binafsi ni mhanga wa matukio haya, niliwahi kupoteza ndugu yangu wa karibu kwenye mafuriko yaliyopiga mikoa ya kusini mwa Tanzania. Ndio! Nakiri mimi ni muathirika kwasababu wazazi wangu waliwahi kupata hasara ya shillingi milioni 4 walizowekeza kwenye kilimo na kutokana na hali ya hewa kutotabirika, hawakuvuna wala kuona faida. Wakulima wanasema kuwa “hela yote imeishia shambani” kutokana na hasara hii, uchumi wa familia uliyumba, nilipata ugumu wa kusoma na kupata mahitaji yangu, na ilichukua takribani miezi sita kwa familia kusimama tena. Unafikiri nini kilichosababisha hasara ile na kutoona mavuno? Mbegu zilizopandwa zilikuwa bora, kanuni za kilimo zote zilifuatwa, kilicholeta hasara ni kukosekana kwa mvua, mabadiliko haya ya tabia nchi sio tu kwamba yaliathiri familia yetu, ila yaliathiri maelfu ya watu wengi ambao wanategemea kilimo kujikimu, kulisha familia zao na kuendesha maisha ya kila siku. Inasikitisha sana!
Kila mtu anapenda amani, hatuwezi kuongelea maendeleo bila amani, lakini vita na vurugu zingine zinatokea katika jamii zetu zinachangiwa na mabadiliko ya tabia nchi. Nimesoma habari za mkoa mmoja unaoitwa Karamoja ambao upo Kaskazini Mashariki mwa nchi ya Uganda, ikipakana na Kenya upande wa Mashariki na Sudan ya Kusini upande wa Kaskazini, eneo hili lina uhaba mkubwa wa chakula hata kusababisha wanajamii wake kutumia nguvu, silaha na ubabe kufaidi rasilimali kidogo ambazo zinapatikana. Eneo hili lina migogoro kwasababu watu waishio hapa wana uhaba wa chakula na wanapambana hata kwa vita kupata malisho kwaajili yao na mifugo yao. Huwa tunasikia vita vya wakulima na wafugaji, moja ya kichocheo cha vita hizi sio tu uhaba wa rasilimali ardhi, lakini pia uhaba wa mazao kwa wakulima na chakula cha mifugo kwa wafugaji, sambamba na hilo, uhaba wa maji yatakayotumika kwenye umwagiliaji wa mazao na maji kwaajili ya kunywesha mifugo. Uhaba huu unachangiwa kwa kiasi kikubwa na mabadiliko ya tabia nchi.
Nipo vizuri katika kuyakumbuka matukio, mwaka 2019, msitu mkubwa duniani wa Amazon uliungua kwa moto, toka Januari hadi Agosti 2019, zaidi ya hekta millioni 12 ziliteketezwa na moto. Nikipiga mahesabu ya idadi ya viumbe hai na rasilimali zilizopotea sipati majibu. Nilipata wasaa wa kumuuliza mtaalamu mmoja wa masuala ya mazingira, kuwa dunia inasubiri nini isizime moto huu? Akanijibu kuwa, hakuna fedha za kutosha zilizotengwa kufanya kazi hiyo. Nilishangaa sana, lakini huu ndio uhalisia, nchi zinaongelea kupambana na mabadiliko ya tabia nchi, lakini ni 2% hadi 5% tu ya bajeti za serikali nyingi kila mwaka huwa zinatengwa kwaajili ya kupambana na mabadiliko haya. Nikajiuliza sana, hali hii itakuwa hivi mpaka lini? Tunasema tutachukua hatua, lakini utekelezaji utaanza lini? Je! Vizazi viwili vinavyokuja vitakuta uoto wa asili, hali ya hewa safi na rasilimali za kutosha kwenye dunia hii? Swali hili hadi sasa kwangu limekuwa fumbo kubwa.
Siku moja nilipata mualiko wa kuzungumza kwenye semina ya vijana kujadili mambo mbalimbali yahusuyo malengo 17 ya maendeleo endelevu, nilipewa nafasi ya kuzungumzia kuhusu hatua za kupambana na mabadiliko ya tabia nchi ambayo ni lengo la 13 la maendeleo endelevu. Niliona huu ni wakati sahihi wa kuhamasisha vijana wajiingize kwenye mapambano haya, wamekuwa nyuma ilihali wao ni waathirika wakubwa. Niliwaeleza vijana kuwa wana wajibu wa kuja na mikakati na mapendekezo ya namna ya kupambana na mabadiliko ya tabia nchi. Dunia inataka kuona vijana wenye mawazo ya kibiashara ya kutunza mazingira, tunatamani kuona vijana wakianzisha mashirika na vikundi vyenye kutetea utunzaji wa mazingira. Nilisisitiza mambo kadhaa yakiwemo yafuatayo;
Sasa hivi zipo fursa kwenye utokomezaji wa bidhaa za plastiki, vijana fungueni macho muone, la zaidi, uchafu wa plastiki umezagaa sana, na unaweza kutumika kutengeneza bidhaa zingine mpya kama matofali, maeneo ya kukaa (yaani mabenchi ya plastiki) n.k. hizi ndio fursa za kujikwamua kiuchumi. Vijana tunapaswa kuelewa kuwa dunia inapiga vita utumiaji wa nishati zisizo rafiki kwa mazingira, tuumize vichwa kujua jinsi gani nishati mbadala zitakavyofika kwenye jamii zetu. Mkataba wa Paris unaelekeza kuweka ukomo wa joto la dunia kutofika nyuzi joto 1.5˚C, na mkakati mojawapo ni kuhakikisha nishati mbadala zinafika maeneo yote, viwanda vinapunguza uchafuzi wa mazingira na teknolojia inatumika kuhakikisha nchi zote zina uwezo wa kupambana na mabadiliko ya tabia nchi.
Wakati nikiendelea kutoa semina ambayo nilizungumzia mambo mengi, ulifika wakati wa maswali. Mshiriki mmoja akaniuliza, “Vijana wana changamoto ya ajira, je! Utawasaidia vipi? Na ni kwa namna gani mapambano ya mabadiliko ya tabia nchi yanavyoweza kufungua fursa za ajira kwa vijana?” Nililipenda sana swali lile, kwani linaakisi maisha ya jamii zetu. Nilijiandaa kutoa majibu ya swali hilo kwa kurejea mkataba wa Paris wa 2015 ambao ulijitengeneza kwenye mikakati mikuu mitatu, katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi, Mkataba wa Paris umebainisha teknolojia, rasilimali fedha na mpango wa kuwajengea uwezo watu kama njia stahiki za kuhakikisha malengo yanafikiwa. Dunia ilifikia maridhiano kuwa nchi zilizoendelea zinapaswa kutoa walau Dola za kimarekani billioni 100 kila mwaka kwaajili ya kusaidia nchi zinazoendelea kupambana na mabadiliko ya tabia nchi.
Rasilimali fedha hizi zinapotolewa zipo ambazo zitawagusa vijana, mfano, kwa kuwapa mitaji na mikopo ili kuanzisha na kuendeleza biashara ambazo zinalenga kutunza mazingira, lakini pia fedha hizi zitajikita katika kuwekeza teknolojia safi na endelevu ambayo itatumika kwenye shughuli mbalimbali za kibinadamu, na teknolojia hizi kwa kiasi kikubwa zinahitaji vijana ambao kwanza watajengewa uwezo wa namna ya kutumia teknolojia hizi. Mfano; katika kuhakikisha kuwa teknolojia inatumika kupambana na madhara ya mabadiliko ya tabia nchi, nchi za Msumbiji, Zimbabwe na Afrika Kusini zilitumia ndege zisizo na rubani (droni) kusambaza taarifa, kupeleka misaada ya chakula n.k kwa wahanga wa kimbunga kikali kilichoambatana na mvua mnamo Januari, 2021. Vijana wachangamke watafute ujuzi wa kutumia teknolojia hizi, ni fursa nzuri sana kwao, kwasababu dunia sasa ni ya kidijitali.
Wakati nahitimisha mafunzo katika semina ile, muda wa mengineyo, nilifurahishwa sana na binti mmoja ambae alisimama na kuelezea ubunifu wake na mambo anayofanya na jinsi ambavyo yamemsaidia na kuisaidia jamii yake kwa ujumla. Binti yule ana ulemavu wa miguu, anatumia viti vya matairi kutembelea, lakini bado anafanya mengi kwenye jamii yake. Binti huyu amebuni programu ya simu ambayo inatoa elimu ya mabadiliko ya tabia nchi, programu yake imejikita katika kuwasaidia watu wenye ulemavu wa kusikia kujifunza zaidi namna wanaweza kushiriki katika kutunza mazingira na kuwa mabalozi wa malengo 17 ya maendeleo endelevu. Programu hii inatoa pia ushauri kwa wakulima juu ya misimu ya kupanda na kuvuna na utabiri wa hali ya hewa ili wawe na uwezo wa kujua yapi yafanyike na kwa wakati gani. Nilimpongeza dada yule na kutamani nipate wasaa zaidi wa kuzungumza nae tuone jinsi wazo lake linavyoweza kukuzwa, na apate pia msaada wa kuendeleza ndoto yake iguse wengi.
Ndoto yangu ni kuona vijana wanakuwa mstari wa mbele kupambana na mabadiliko ya tabia nchi, ni wakati ambao haitoshi tu kuwafanya vijana kama sehemu ya matatizo katika jamii, lakini ni vyema zaidi vijana wakatumika kama sehemu ya utatuzi wa matatizo yaliyoko katika jamii. Vijana tunaweza, tunapaswa kushirikishwa kwenye mapambano haya, ni haki yetu, na wakati sahihi ni sasa!
About
Humphrey W. Mrema is a young leader, equipped with skills and experience of leadership in the community. He co-founded Youth Survival Organization, which has impacted more than 5,000 youths since 2018 by providing education on SDGs, promoting talents, doing charitable works, and volunteerism advocacy.
He also works with other NGOs and Associates in Tanzania and abroad, including Global Shapers Community, Peace First, and Women in Management Africa, International Christian Youthworks, Restless Development, and UN Climate Change Conference of Youth (COY16) Global Affairs Unit (GAU). Currently, he is the Chairman of the Youth Survival Organization and Tanzanian Country coordinator for the UN Climate Change Conference of Youth (COY16). In the area of expertise, Humphrey is an Urban Planning Student at Ardhi University, Dar es Salaam, expecting to complete his Bachelor's degree of Science in Urban and Regional Planning later in 2022.